Zaburi Mlango 119 Psalms

Zaburi 119:1

Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.

Zaburi 119:2

Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote.

Zaburi 119:3

Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake.

Zaburi 119:4

Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana.

Zaburi 119:5

Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako.

Zaburi 119:6

Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote.

Zaburi 119:7

Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako

Zaburi 119:8

Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa

Zaburi 119:9

Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.

Zaburi 119:10

Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.

Zaburi 119:11

Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.

Zaburi 119:12

Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako.

Zaburi 119:13

Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako.

Zaburi 119:14

Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi.

Zaburi 119:15

Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako.

Zaburi 119:16

Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako.

Zaburi 119:17

Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.

Zaburi 119:18

Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.

Zaburi 119:19

Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako.

Zaburi 119:20

Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati.

Zaburi 119:21

Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.

Zaburi 119:22

Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako.

Zaburi 119:23

Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.

Zaburi 119:24

Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu.

Zaburi 119:25

Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.

Zaburi 119:26

Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako.

Zaburi 119:27

Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako.

Zaburi 119:28

Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.

Zaburi 119:29

Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako.

Zaburi 119:30

Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.

Zaburi 119:31

Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe.

Zaburi 119:32

Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu.

Zaburi 119:33

Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho.

Zaburi 119:34

Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.

Zaburi 119:35

Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo.

Zaburi 119:36

Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa.

Zaburi 119:37

Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako.

Zaburi 119:38

Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako.

Zaburi 119:39

Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema.

Zaburi 119:40

Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako.

Zaburi 119:41

Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.

Zaburi 119:42

Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako.

Zaburi 119:43

Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako.

Zaburi 119:44

Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele.

Zaburi 119:45

Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.

Zaburi 119:46

Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu.

Zaburi 119:47

Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.

Zaburi 119:48

Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.

Zaburi 119:49

Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha.

Zaburi 119:50

Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.

Zaburi 119:51

Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako.

Zaburi 119:52

Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji.

Zaburi 119:53

Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako.

Zaburi 119:54

Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu.

Zaburi 119:55

Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako.

Zaburi 119:56

Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.

Zaburi 119:57

Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.

Zaburi 119:58

Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako.

Zaburi 119:59

Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.

Zaburi 119:60

Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako.

Zaburi 119:61

Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.

Zaburi 119:62

Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki.

Zaburi 119:63

Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako.

Zaburi 119:64

Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.

Zaburi 119:65

Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako.

Zaburi 119:66

Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.

Zaburi 119:67

Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako.

Zaburi 119:68

Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako.

Zaburi 119:69

Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.

Zaburi 119:70

Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako.

Zaburi 119:71

Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.

Zaburi 119:72

Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

Zaburi 119:73

Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako.

Zaburi 119:74

Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako.

Zaburi 119:75

Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.

Zaburi 119:76

Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.

Zaburi 119:77

Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu.

Zaburi 119:78

Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako.

Zaburi 119:79

Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako.

Zaburi 119:80

Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.

Zaburi 119:81

Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako.

Zaburi 119:82

Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji?

Zaburi 119:83

Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako.

Zaburi 119:84

Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?

Zaburi 119:85

Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako.

Zaburi 119:86

Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie.

Zaburi 119:87

Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako.

Zaburi 119:88

Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.

Zaburi 119:89

Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele.

Zaburi 119:90

Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.

Zaburi 119:91

Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.

Zaburi 119:92

Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu.

Zaburi 119:93

Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha.

Zaburi 119:94

Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako.

Zaburi 119:95

Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako.

Zaburi 119:96

Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno.

Zaburi 119:97

Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.

Zaburi 119:98

Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote.

Zaburi 119:99

Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.

Zaburi 119:100

Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.

Zaburi 119:101

Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako.

Zaburi 119:102

Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.

Zaburi 119:103

Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu.

Zaburi 119:104

Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.

Zaburi 119:105

Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.

Zaburi 119:106

Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.

Zaburi 119:107

Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako.

Zaburi 119:108

Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako.

Zaburi 119:109

Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau.

Zaburi 119:110

Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.

Zaburi 119:111

Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu.

Zaburi 119:112

Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele.

Zaburi 119:113

Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda.

Zaburi 119:114

Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea.

Zaburi 119:115

Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu.

Zaburi 119:116

Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.

Zaburi 119:117

Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima.

Zaburi 119:118

Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo.

Zaburi 119:119

Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.

Zaburi 119:120

Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako.

Zaburi 119:121

Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea.

Zaburi 119:122

Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee.

Zaburi 119:123

Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako.

Zaburi 119:124

Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe.

Zaburi 119:125

Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako.

Zaburi 119:126

Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.

Zaburi 119:127

Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.

Zaburi 119:128

Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia.

Zaburi 119:129

Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.

Zaburi 119:130

Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.

Zaburi 119:131

Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako.

Zaburi 119:132

Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.

Zaburi 119:133

Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki.

Zaburi 119:134

Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako.

Zaburi 119:135

Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako.

Zaburi 119:136

Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako.

Zaburi 119:137

Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.

Zaburi 119:138

Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.

Zaburi 119:139

Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.

Zaburi 119:140

Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.

Zaburi 119:141

Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako.

Zaburi 119:142

Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli.

Zaburi 119:143

Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu.

Zaburi 119:144

Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi.

Zaburi 119:145

Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako.

Zaburi 119:146

Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako.

Zaburi 119:147

Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini.

Zaburi 119:148

Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako.

Zaburi 119:149

Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako.

Zaburi 119:150

Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako.

Zaburi 119:151

Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli.

Zaburi 119:152

Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele.

Zaburi 119:153

Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako.

Zaburi 119:154

Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako.

Zaburi 119:155

Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.

Zaburi 119:156

Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako.

Zaburi 119:157

Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.

Zaburi 119:158

Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako.

Zaburi 119:159

Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako.

Zaburi 119:160

Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.

Zaburi 119:161

Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako.

Zaburi 119:162

Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi.

Zaburi 119:163

Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda.

Zaburi 119:164

Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako.

Zaburi 119:165

Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.

Zaburi 119:166

Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda.

Zaburi 119:167

Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno.

Zaburi 119:168

Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako.

Zaburi 119:169

Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako.

Zaburi 119:170

Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako.

Zaburi 119:171

Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.

Zaburi 119:172

Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki.

Zaburi 119:173

Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako.

Zaburi 119:174

Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu.

Zaburi 119:175

Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie.

Zaburi 119:176

Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.