Zaburi Mlango 81 Psalms

Zaburi 81:1

Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo.

Zaburi 81:2

Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.

Zaburi 81:3

Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu.

Zaburi 81:4

Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.

Zaburi 81:5

Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.

Zaburi 81:6

Nimelitenga bega lake na mzigo, Mikono yake ikaachana na kikapu.

Zaburi 81:7

Katika shida uliniita nikakuokoa; Nalikuitikia katika sitara ya radi; Nalikujaribu penye maji ya Meriba.

Zaburi 81:8

Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya, Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza;

Zaburi 81:9

Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine.

Zaburi 81:10

Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.

Zaburi 81:11

Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka.

Zaburi 81:12

Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao.

Zaburi 81:13

Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu;

Zaburi 81:14

Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;

Zaburi 81:15

Wamchukiao Bwana wangenyenyekea mbele zake, Bali wakati wao ungedumu milele.

Zaburi 81:16

Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.