Zaburi Mlango 34 Psalms

Zaburi 34:1

Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.

Zaburi 34:2

Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

Zaburi 34:3

Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.

Zaburi 34:4

Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.

Zaburi 34:5

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.

Zaburi 34:6

Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.

Zaburi 34:7

Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.

Zaburi 34:8

Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.

Zaburi 34:9

Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.

Zaburi 34:10

Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.

Zaburi 34:11

Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.

Zaburi 34:12

Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema?

Zaburi 34:13

Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.

Zaburi 34:14

Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.

Zaburi 34:15

Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao.

Zaburi 34:16

Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.

Zaburi 34:17

Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.

Zaburi 34:18

Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.

Zaburi 34:19

Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.

Zaburi 34:20

Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.

Zaburi 34:21

Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.

Zaburi 34:22

Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.