Zaburi Mlango 68 Psalms

Zaburi 68:1

Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake.

Zaburi 68:2

Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu.

Zaburi 68:3

Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha.

Zaburi 68:4

Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake.

Zaburi 68:5

Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu.

Zaburi 68:6

Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.

Zaburi 68:7

Ee Mungu, ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani,

Zaburi 68:8

Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli.

Zaburi 68:9

Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.

Zaburi 68:10

Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.

Zaburi 68:11

Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;

Zaburi 68:12

Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia; Na mwanamke akaaye nyumbani agawa nyara.

Zaburi 68:13

Kwa nini kulala mazizini arukapo hua, Mbawa zake ziking'aa kama fedha Na manyoya yake kama dhahabu?

Zaburi 68:14

Mwenyezi Mungu alipotawanya wafalme huko, Kulinyesha theluji katika Salmoni.

Zaburi 68:15

Ni mlima wa Mungu mlima Bashani, Ni mlima mrefu mlima Bashani.

Zaburi 68:16

Enyi milima mirefu, kwani kuutazama kwa wivu Mlima alioutamani Mungu akae juu yake? Naam, Bwana atakaa juu yake milele.

Zaburi 68:17

Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu.

Zaburi 68:18

Wewe umepaa juu, umeteka mateka, Umepewa vipawa katikati ya wanadamu; Naam, hata na wakaidi, Bwana Mungu akae nao.

Zaburi 68:19

Na ahimidiwe Bwana, Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu.

Zaburi 68:20

Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.

Zaburi 68:21

Naam, Mungu atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afulizaye kukosa.

Zaburi 68:22

Bwana alisema, Kutoka Bashani nitawarudisha, Nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari;

Zaburi 68:23

Uuchovye mguu wako katika damu ya adui zako, Na ulimi wa mbwa zako upate sehemu yake.

Zaburi 68:24

Ee Mungu, wameiona miendo yako; Miendo ya Mungu wangu, Mfalme wangu, katika patakatifu

Zaburi 68:25

Waimbaji hutangulia, nyuma yao wapigao vinanda, Kati ya wanawali wapiga matari.

Zaburi 68:26

Mhimidini Mungu katika mikutano, Bwana katika makusanyiko ya Israeli.

Zaburi 68:27

Yuko Benyamini mdogo, mtawala wao; Wakuu wa Yuda, kundi lao; Wakuu wa Zabuloni; Wakuu wa Naftali.

Zaburi 68:28

Ee Mungu, uziamuru nguvu zako; Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.

Zaburi 68:29

Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu Wafalme watakuletea hedaya.

Zaburi 68:30

Mkemee mnyama wa manyasini; Kundi la mafahali, na ndama za watu; Hata wanyenyekee na kuleta vipande vya fedha, Uwatawanye watu wapendao vita.

Zaburi 68:31

Masheki watakuja kutoka Misri, Kushi itamnyoshea Mungu mikono yake mara.

Zaburi 68:32

Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu, Msifuni Bwana kwa nyimbo.

Zaburi 68:33

Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele; Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.

Zaburi 68:34

Mhesabieni Mungu nguvu; Enzi yake i juu ya Israeli; Na nguvu zake zi mawinguni.

Zaburi 68:35

Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako. Ndiye Mungu wa Israeli; Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo. Na ahimidiwe Mungu.