Zaburi Mlango 62 Psalms

Zaburi 62:1

Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake.

Zaburi 62:2

Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.

Zaburi 62:3

Hata lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama kitalu kilicho tayari kuanguka,

Zaburi 62:4

Hufanya shauri kumwangusha tu katika cheo chake; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani.

Zaburi 62:5

Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake.

Zaburi 62:6

Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.

Zaburi 62:7

Kwa Mungu wokovu wangu, Na utukufu wangu; Mwamba wa nguvu zangu, Na kimbilio langu ni kwa Mungu.

Zaburi 62:8

Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.

Zaburi 62:9

Hakika binadamu ni ubatili, Na wenye cheo ni uongo, Katika mizani huinuka; Wote pamoja ni hafifu kuliko ubatili.

Zaburi 62:10

Msiitumainie dhuluma, Wala msijivune kwa unyang'anyi; Mali izidipo msiiangalie sana moyoni.

Zaburi 62:11

Mara moja amenena Mungu; Mara mbili nimeyasikia haya, Ya kuwa nguvu zina Mungu,

Zaburi 62:12

Na fadhili ziko kwako, Ee Bwana; Maana ndiwe umlipaye kila mtu Sawasawa na haki yake.