Zaburi Mlango 28 Psalms

Zaburi 28:1

Ee Bwana, nitakuita Wewe, mwamba wangu, Usiwe kwangu kama kiziwi. Nisije nikafanana nao washukao shimoni, Ikiwa umeninyamalia.

Zaburi 28:2

Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, Nikipainulia patakatifu pako mikono yangu.

Zaburi 28:3

Usinikokote pamoja na wasio haki, Wala pamoja na watenda maovu. Wawaambiao jirani zao maneno ya amani, Lakini mioyoni mwao mna madhara.

Zaburi 28:4

Uwape sawasawa na vitendo vyao, Na kwa kadiri ya ubaya wa kufanya kwao, Uwape sawasawa na kazi ya mikono yao, Uwalipe stahili zao.

Zaburi 28:5

Maana hawazifahamu kazi za Bwana, Wala matendo ya mikono yake. Atawavunja wala hatawajenga;

Zaburi 28:6

Na ahimidiwe Bwana. Maana ameisikia sauti ya dua yangu;

Zaburi 28:7

Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru.

Zaburi 28:8

Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake.

Zaburi 28:9

Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, Uwachunge, uwachukue milele.