Zaburi Mlango 33 Psalms

Zaburi 33:1

Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

Zaburi 33:2

Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

Zaburi 33:3

Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.

Zaburi 33:4

Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.

Zaburi 33:5

Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.

Zaburi 33:6

Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.

Zaburi 33:7

Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala.

Zaburi 33:8

Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche.

Zaburi 33:9

Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.

Zaburi 33:10

Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu.

Zaburi 33:11

Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.

Zaburi 33:12

Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

Zaburi 33:13

Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia.

Zaburi 33:14

Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani.

Zaburi 33:15

yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote.

Zaburi 33:16

Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu.

Zaburi 33:17

Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.

Zaburi 33:18

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.

Zaburi 33:19

Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.

Zaburi 33:20

Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.

Zaburi 33:21

Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.

Zaburi 33:22

Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.