Zaburi Mlango 41 Psalms

Zaburi 41:1

Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu.

Zaburi 41:2

Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake.

Zaburi 41:3

Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.

Zaburi 41:4

Nami nalisema, Bwana, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi.

Zaburi 41:5

Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea?

Zaburi 41:6

Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena.

Zaburi 41:7

Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.

Zaburi 41:8

Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena.

Zaburi 41:9

Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.

Zaburi 41:10

Lakini Wewe, Bwana, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa.

Zaburi 41:11

Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hasimangi kwa kunishinda.

Zaburi 41:12

Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele.

Zaburi 41:13

Na atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.