Zaburi Mlango 5 Psalms

Zaburi 5:1

Ee Bwana, uyasikilize maneno yangu, Ukuangalie kutafakari kwangu.

Zaburi 5:2

Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.

Zaburi 5:3

Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.

Zaburi 5:4

Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako;

Zaburi 5:5

Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao ubatili.

Zaburi 5:6

Utawaharibu wasemao uongo; Bwana humzira mwuaji na mwenye hila

Zaburi 5:7

Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu.

Zaburi 5:8

Bwana, uniongoze kwa haki yako, Kwa sababu yao wanaoniotea. Uisawazishe njia yako mbele ya uso wangu,

Zaburi 5:9

Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Mtima wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza.

Zaburi 5:10

Wewe, Mungu, uwapatilize, Na waanguke kwa mashauri yao. Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, Kwa maana wamekuasi Wewe.

Zaburi 5:11

Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia.

Zaburi 5:12

Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; Bwana, utamzungushia radhi kama ngao.