Zaburi Mlango 37 Psalms

Zaburi 37:1

Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili.

Zaburi 37:2

Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka.

Zaburi 37:3

Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.

Zaburi 37:4

Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.

Zaburi 37:5

Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.

Zaburi 37:6

Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri.

Zaburi 37:7

Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila.

Zaburi 37:8

Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.

Zaburi 37:9

Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi.

Zaburi 37:10

Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.

Zaburi 37:11

Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani.

Zaburi 37:12

Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake.

Zaburi 37:13

Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.

Zaburi 37:14

Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu.

Zaburi 37:15

Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika.

Zaburi 37:16

Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi.

Zaburi 37:17

Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali Bwana huwategemeza wenye haki.

Zaburi 37:18

Bwana anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele.

Zaburi 37:19

Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba.

Zaburi 37:20

Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao Bwana watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka.

Zaburi 37:21

Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.

Zaburi 37:22

Maana waliobarikiwa na yeye watairithi nchi, Nao waliolaaniwa na yeye wataharibiwa.

Zaburi 37:23

Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake.

Zaburi 37:24

Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza.

Zaburi 37:25

Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.

Zaburi 37:26

Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa.

Zaburi 37:27

Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele.

Zaburi 37:28

Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.

Zaburi 37:29

Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele.

Zaburi 37:30

Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu.

Zaburi 37:31

Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi.

Zaburi 37:32

Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha.

Zaburi 37:33

Bwana hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa.

Zaburi 37:34

Wewe umngoje Bwana, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona.

Zaburi 37:35

Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni.

Zaburi 37:36

Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana.

Zaburi 37:37

Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.

Zaburi 37:38

Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa.

Zaburi 37:39

Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.

Zaburi 37:40

Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.