Zaburi Mlango 72 Psalms

Zaburi 72:1

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, Na mwana wa mfalme haki yako.

Zaburi 72:2

Atawaamua watu wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

Zaburi 72:3

Milima itawazalia watu amani, Na vilima navyo kwa haki.

Zaburi 72:4

Atawahukumu walioonewa wa watu, Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea.

Zaburi 72:5

Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua, Na wakati wa kung'aa mwezi kizazi hata kizazi.

Zaburi 72:6

Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa, Kama manyunyu yainyweshayo nchi.

Zaburi 72:7

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Zaburi 72:8

Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia.

Zaburi 72:9

Wakaao jangwani na wainame mbele zake; Adui zake na warambe mavumbi.

Zaburi 72:10

Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.

Zaburi 72:11

Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie.

Zaburi 72:12

Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.

Zaburi 72:13

Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa.

Zaburi 72:14

Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, Na damu yao ina thamani machoni pake.

Zaburi 72:15

Basi na aishi; Na wampe dhahabu ya Sheba; Na wamwombee daima; Na kumbariki mchana kutwa.

Zaburi 72:16

Na uwepo wingi wa nafaka Katika ardhi juu ya milima; Matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni, Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.

Zaburi 72:17

Jina lake na lidumu milele, Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao; Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri.

Zaburi 72:18

Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Mungu wa Israeli, Atendaye miujiza Yeye peke yake;

Zaburi 72:19

Jina lake tukufu na lihimidiwe milele; Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.

Zaburi 72:20

Maombi ya Daudi mwana wa Yese yamekwisha.