Zaburi Mlango 139 Psalms

Zaburi 139:1

Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.

Zaburi 139:2

Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.

Zaburi 139:3

Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.

Zaburi 139:4

Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.

Zaburi 139:5

Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako.

Zaburi 139:6

Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.

Zaburi 139:7

Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?

Zaburi 139:8

Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.

Zaburi 139:9

Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari;

Zaburi 139:10

Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.

Zaburi 139:11

Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;

Zaburi 139:12

Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.

Zaburi 139:13

Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.

Zaburi 139:14

Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,

Zaburi 139:15

Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi;

Zaburi 139:16

Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.

Zaburi 139:17

Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake!

Zaburi 139:18

Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.

Zaburi 139:19

Ee Mungu, laiti ungewafisha waovu! Enyi watu wa damu, ondokeni kwangu;

Zaburi 139:20

Kwa maana wakuasi kwa ubaya, Adui zako wakutaja jina lako bure.

Zaburi 139:21

Je! Bwana nisiwachukie wanaokuchukia? Nisikirihike nao wakuasio?

Zaburi 139:22

Nawachukia kwa ukomo wa chuki, Wamekuwa adui kwangu.

Zaburi 139:23

Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;

Zaburi 139:24

Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.