Zaburi Mlango 103 Psalms

Zaburi 103:1

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.

Zaburi 103:2

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.

Zaburi 103:3

Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,

Zaburi 103:4

Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,

Zaburi 103:5

Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;

Zaburi 103:6

Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa.

Zaburi 103:7

Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.

Zaburi 103:8

Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.

Zaburi 103:9

Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele.

Zaburi 103:10

Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.

Zaburi 103:11

Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.

Zaburi 103:12

Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.

Zaburi 103:13

Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.

Zaburi 103:14

Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.

Zaburi 103:15

Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.

Zaburi 103:16

Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.

Zaburi 103:17

Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana;

Zaburi 103:18

Maana, wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.

Zaburi 103:19

Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.

Zaburi 103:20

Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.

Zaburi 103:21

Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.

Zaburi 103:22

Mhimidini Bwana, enyi matendo yake yote, Mahali pote pa milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.