Zaburi Mlango 78 Psalms

Zaburi 78:1

Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.

Zaburi 78:2

Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale.

Zaburi 78:3

Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia.

Zaburi 78:4

Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za Bwana, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya.

Zaburi 78:5

Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao,

Zaburi 78:6

Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao

Zaburi 78:7

Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake.

Zaburi 78:8

Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.

Zaburi 78:9

Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita.

Zaburi 78:10

Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake;

Zaburi 78:11

Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha.

Zaburi 78:12

Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani.

Zaburi 78:13

Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu.

Zaburi 78:14

Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto.

Zaburi 78:15

Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi.

Zaburi 78:16

Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito.

Zaburi 78:17

Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu.

Zaburi 78:18

Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.

Zaburi 78:19

Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani?

Zaburi 78:20

Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama?

Zaburi 78:21

Hivyo Bwana aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli.

Zaburi 78:22

Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake.

Zaburi 78:23

Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni;

Zaburi 78:24

Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni.

Zaburi 78:25

Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.

Zaburi 78:26

Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake.

Zaburi 78:27

Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari.

Zaburi 78:28

Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao.

Zaburi 78:29

Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani;

Zaburi 78:30

Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao

Zaburi 78:31

Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli.

Zaburi 78:32

Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.

Zaburi 78:33

Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha.

Zaburi 78:34

Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.

Zaburi 78:35

Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao.

Zaburi 78:36

Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.

Zaburi 78:37

Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.

Zaburi 78:38

Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote.

Zaburi 78:39

Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi.

Zaburi 78:40

Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani!

Zaburi 78:41

Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.

Zaburi 78:42

Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi.

Zaburi 78:43

Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani.

Zaburi 78:44

Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa.

Zaburi 78:45

Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu.

Zaburi 78:46

Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao.

Zaburi 78:47

Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.

Zaburi 78:48

Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme.

Zaburi 78:49

Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya.

Zaburi 78:50

Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;

Zaburi 78:51

Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.

Zaburi 78:52

Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani.

Zaburi 78:53

Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao.

Zaburi 78:54

Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume.

Zaburi 78:55

Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.

Zaburi 78:56

Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake.

Zaburi 78:57

Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa.

Zaburi 78:58

Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao.

Zaburi 78:59

Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa.

Zaburi 78:60

Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;

Zaburi 78:61

Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi.

Zaburi 78:62

Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake.

Zaburi 78:63

Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,

Zaburi 78:64

Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza.

Zaburi 78:65

Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;

Zaburi 78:66

Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele.

Zaburi 78:67

Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu.

Zaburi 78:68

Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda.

Zaburi 78:69

Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele.

Zaburi 78:70

Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo.

Zaburi 78:71

Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake.

Zaburi 78:72

Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.