Zaburi Mlango 108 Psalms

Zaburi 108:1

Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Nitaimba, nitaimba zaburi, Naam, kwa utukufu wangu.

Zaburi 108:2

Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.

Zaburi 108:3

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.

Zaburi 108:4

Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni.

Zaburi 108:5

Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.

Zaburi 108:6

Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono wako wa kuume, uniitikie.

Zaburi 108:7

Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi.

Zaburi 108:8

Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,

Zaburi 108:9

Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.

Zaburi 108:10

Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hata Edomu?

Zaburi 108:11

Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu?

Zaburi 108:12

Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai.

Zaburi 108:13

Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.