Zaburi Mlango 84 Psalms

Zaburi 84:1

Maskani zako zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi!

Zaburi 84:2

Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana, Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai.

Zaburi 84:3

Shomoro naye ameona nyumba, Na mbayuwayu amejipatia kioto, Alipoweka makinda yake, Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu.

Zaburi 84:4

Heri wakaao nyumbani mwako, Wanakuhimidi daima.

Zaburi 84:5

Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.

Zaburi 84:6

Wakipita kati ya bonde la Vilio, Hulifanya kuwa chemchemi, Naam, mvua ya vuli hulivika baraka

Zaburi 84:7

Huendelea toka nguvu hata nguvu, Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.

Zaburi 84:8

Bwana, Mungu wa majeshi, uyasikie maombi yangu, Ee Mungu wa Yakobo, usikilize,

Zaburi 84:9

Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, Umtazame uso masihi wako.

Zaburi 84:10

Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu.

Zaburi 84:11

Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.

Zaburi 84:12

Ee Bwana wa majeshi, Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.