Zaburi Mlango 10 Psalms

Zaburi 10:1

Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?

Zaburi 10:2

Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.

Zaburi 10:3

Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.

Zaburi 10:4

Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu;

Zaburi 10:5

Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya.

Zaburi 10:6

Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.

Zaburi 10:7

Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,

Zaburi 10:8

Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni.

Zaburi 10:9

Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake.

Zaburi 10:10

Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake.

Zaburi 10:11

Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.

Zaburi 10:12

Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge.

Zaburi 10:13

Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza?

Zaburi 10:14

Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima.

Zaburi 10:15

Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione.

Zaburi 10:16

Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake.

Zaburi 10:17

Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako.

Zaburi 10:18

Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.