Zaburi Mlango 71 Psalms

Zaburi 71:1

Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele.

Zaburi 71:2

Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe.

Zaburi 71:3

Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.

Zaburi 71:4

Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu,

Zaburi 71:5

Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu.

Zaburi 71:6

Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima.

Zaburi 71:7

Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.

Zaburi 71:8

Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa.

Zaburi 71:9

Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.

Zaburi 71:10

Kwa maana adui zangu wananiamba, Nao wanaoniotea roho yangu hushauriana.

Zaburi 71:11

Wakisema, Mungu amemwacha, Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya.

Zaburi 71:12

Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.

Zaburi 71:13

Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.

Zaburi 71:14

Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote.

Zaburi 71:15

Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.

Zaburi 71:16

Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.

Zaburi 71:17

Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.

Zaburi 71:18

Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako.

Zaburi 71:19

Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

Zaburi 71:20

Wewe, uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya, Utatuhuisha tena. Utatupandisha juu tena Tokea pande za chini ya nchi.

Zaburi 71:21

Laiti ungeniongezea ukuu! Urejee tena na kunifariji moyo.

Zaburi 71:22

Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu. Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli.

Zaburi 71:23

Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, Na nafsi yangu uliyoikomboa.

Zaburi 71:24

Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.