Zaburi Mlango 135 Psalms

Zaburi 135:1

Haleluya. Lisifuni jina la Bwana, Enyi watumishi wa Bwana, sifuni.

Zaburi 135:2

Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu.

Zaburi 135:3

Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema, Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza.

Zaburi 135:4

Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa.

Zaburi 135:5

Maana najua mimi ya kuwa Bwana ni mkuu, Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote.

Zaburi 135:6

Bwana amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote.

Zaburi 135:7

Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi; Huifanyia mvua umeme; Hutoa upepo katika hazina zake.

Zaburi 135:8

Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, Wa wanadamu na wa wanyama.

Zaburi 135:9

Alipeleka ishara na maajabu kati yako, Ee Misri, Juu ya Farao na watumishi wake wote.

Zaburi 135:10

Aliwapiga mataifa mengi, Akawaua wafalme wenye nguvu;

Zaburi 135:11

Sihoni, mfalme wa Waamori, Na Ogu, mfalme wa Bashani, Na falme zote za Kanaani.

Zaburi 135:12

Akaitoa nchi yao iwe urithi, Urithi wa Israeli watu wake.

Zaburi 135:13

Ee Bwana, jina lako ni la milele, Bwana, kumbukumbu lako vizazi hata vizazi.

Zaburi 135:14

Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumishi wake.

Zaburi 135:15

Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.

Zaburi 135:16

Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,

Zaburi 135:17

Zina masikio lakini hazisikii, Wala hamna pumzi vinywani mwake.

Zaburi 135:18

Wazifanyao watafanana nazo, Na kila mmoja anayezitumainia.

Zaburi 135:19

Enyi mlango wa Israeli, mhimidini Bwana; Enyi mlango wa Haruni, mhimidini Bwana;

Zaburi 135:20

Enyi mlango wa Lawi, mhimidini Bwana; Ninyi mnaomcha Bwana, mhimidini Bwana.

Zaburi 135:21

Na ahimidiwe Bwana toka Sayuni, Akaaye Yerusalemu. Haleluya.