Zaburi Mlango 118 Psalms

Zaburi 118:1

Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Zaburi 118:2

Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

Zaburi 118:3

Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

Zaburi 118:4

Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

Zaburi 118:5

Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi.

Zaburi 118:6

Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?

Zaburi 118:7

Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa.

Zaburi 118:8

Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu.

Zaburi 118:9

Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu.

Zaburi 118:10

Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

Zaburi 118:11

Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

Zaburi 118:12

Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

Zaburi 118:13

Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.

Zaburi 118:14

Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.

Zaburi 118:15

Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.

Zaburi 118:16

Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.

Zaburi 118:17

Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.

Zaburi 118:18

Bwana ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife.

Zaburi 118:19

Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru Bwana.

Zaburi 118:20

Lango hili ni la Bwana, Wenye haki ndio watakaoliingia.

Zaburi 118:21

Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu.

Zaburi 118:22

Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

Zaburi 118:23

Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.

Zaburi 118:24

Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

Zaburi 118:25

Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.

Zaburi 118:26

Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.

Zaburi 118:27

Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu.

Zaburi 118:28

Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza.

Zaburi 118:29

Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.