Zaburi Mlango 105 Psalms

Zaburi 105:1

Haleluya. Mshukuruni Bwana,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake.

Zaburi 105:2

Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.

Zaburi 105:3

Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.

Zaburi 105:4

Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote.

Zaburi 105:5

Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya, Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.

Zaburi 105:6

Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.

Zaburi 105:7

Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake.

Zaburi 105:8

Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.

Zaburi 105:9

Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka.

Zaburi 105:10

Alilomthibitishia Yakobo liwe amri, Na Israeli liwe agano la milele.

Zaburi 105:11

Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa.

Zaburi 105:12

Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa, Naam, watu wachache na wageni ndani yake,

Zaburi 105:13

Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine.

Zaburi 105:14

Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.

Zaburi 105:15

Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.

Zaburi 105:16

Akaiita njaa iijilie nchi, Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

Zaburi 105:17

Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani.

Zaburi 105:18

Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.

Zaburi 105:19

Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya Bwana ilimjaribu.

Zaburi 105:20

Mfalme alituma watu akamfungua, Mkuu wa watu akamwachia.

Zaburi 105:21

Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake, Na mwenye amri juu ya mali zake zote.

Zaburi 105:22

Awafunge masheki wake kama apendavyo, Na kuwafundisha wazee wake hekima.

Zaburi 105:23

Israeli naye akaingia Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.

Zaburi 105:24

Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao.

Zaburi 105:25

Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake.

Zaburi 105:26

Akamtuma Musa, mtumishi wake, Na Haruni ambaye amemchagua.

Zaburi 105:27

Akaweka mambo ya ishara zake kati yao, Na miujiza katika nchi ya Hamu.

Zaburi 105:28

Alituma giza, kukafunga giza, Wala hawakuyaasi maneno yake.

Zaburi 105:29

Aliyageuza maji yao yakawa damu, Akawafisha samaki wao.

Zaburi 105:30

Nchi yao ilijaa vyura, Vyumbani mwa wafalme wao.

Zaburi 105:31

Alisema, kukaja makundi ya mainzi, Na chawa mipakani mwao mwote.

Zaburi 105:32

Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe, Na moto wa miali katika nchi yao.

Zaburi 105:33

Akaipiga mizabibu yao na mitini yao, Akaivunja miti ya mipaka yao.

Zaburi 105:34

Alisema, kukaja nzige, Na tunutu wasiohesabika;

Zaburi 105:35

Wakaila miche yote ya nchi yao, Wakayala matunda ya ardhi yao.

Zaburi 105:36

Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi, Malimbuko ya nguvu zao.

Zaburi 105:37

Akawatoa hali wana fedha na dhahabu, Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa.

Zaburi 105:38

Misri ilifurahi walipoondoka, Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia.

Zaburi 105:39

Alitandaza wingu liwe funiko, Na moto utoe nuru usiku.

Zaburi 105:40

Walipotaka akaleta kware, Akawashibisha chakula cha mbinguni.

Zaburi 105:41

Akaufunua mwamba, kukabubujika maji, Yakapita pakavuni kama mto.

Zaburi 105:42

Maana alilikumbuka neno lake takatifu, Na Ibrahimu, mtumishi wake.

Zaburi 105:43

Akawatoa watu wake kwa shangwe, Na wateule wake kwa nyimbo za furaha.

Zaburi 105:44

Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu;

Zaburi 105:45

Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake. Haleluya.