Zaburi Mlango 27 Psalms

Zaburi 27:1

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?

Zaburi 27:2

Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka.

Zaburi 27:3

Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.

Zaburi 27:4

Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.

Zaburi 27:5

Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.

Zaburi 27:6

Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi Bwana.

Zaburi 27:7

Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu.

Zaburi 27:8

Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.

Zaburi 27:9

Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.

Zaburi 27:10

Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake.

Zaburi 27:11

Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;

Zaburi 27:12

Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi.

Zaburi 27:13

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.

Zaburi 27:14

Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.