Zaburi Mlango 44 Psalms

Zaburi 44:1

Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.

Zaburi 44:2

Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao.

Zaburi 44:3

Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia.

Zaburi 44:4

Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.

Zaburi 44:5

Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.

Zaburi 44:6

Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa.

Zaburi 44:7

Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha.

Zaburi 44:8

Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.

Zaburi 44:9

Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu.

Zaburi 44:10

Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka.

Zaburi 44:11

Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa.

Zaburi 44:12

Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao.

Zaburi 44:13

Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

Zaburi 44:14

Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.

Zaburi 44:15

Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika,

Zaburi 44:16

Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.

Zaburi 44:17

Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako.

Zaburi 44:18

Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako.

Zaburi 44:19

Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.

Zaburi 44:20

Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;

Zaburi 44:21

Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo.

Zaburi 44:22

Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa.

Zaburi 44:23

Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa.

Zaburi 44:24

Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?

Zaburi 44:25

Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi.

Zaburi 44:26

Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.