Zaburi Mlango 31 Psalms

Zaburi 31:1

Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,

Zaburi 31:2

Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.

Zaburi 31:3

Ndiwe genge langu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.

Zaburi 31:4

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

Zaburi 31:5

Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.

Zaburi 31:6

Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumaini Bwana.

Zaburi 31:7

Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni,

Zaburi 31:8

Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.

Zaburi 31:9

Ee Bwana, unifadhili, maana ni katika dhiki, Jicho langu limenyauka kwa masumbufu, Naam, mwili wangu na nafsi yangu.

Zaburi 31:10

Maana maisha yangu yamekoma kwa huzuni, Na miaka yangu kwa kuugua. Nguvu zangu zinatetemeka kwa uovu wangu, Na mifupa yangu imekauka.

Zaburi 31:11

Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Walioniona njiani walinikimbia.

Zaburi 31:12

Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.

Zaburi 31:13

Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu.

Zaburi 31:14

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Zaburi 31:15

Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.

Zaburi 31:16

Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.

Zaburi 31:17

Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.

Zaburi 31:18

Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.

Zaburi 31:19

Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao; Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu!

Zaburi 31:20

Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako; Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi.

Zaburi 31:21

Bwana ahimidiwe; kwa maana amenitendea Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.

Zaburi 31:22

Nami nalisema kwa haraka yangu, Nimekatiliwa mbali na macho yako; Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia.

Zaburi 31:23

Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake. Bwana huwahifadhi waaminifu, Humlipa atendaye kiburi malipo tele.

Zaburi 31:24

Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana.