Zaburi Mlango 19 Psalms

Zaburi 19:1

Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.

Zaburi 19:2

Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.

Zaburi 19:3

Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani.

Zaburi 19:4

Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema,

Zaburi 19:5

Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake.

Zaburi 19:6

Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hari yake Hakuna kitu kilichositirika.

Zaburi 19:7

Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.

Zaburi 19:8

Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.

Zaburi 19:9

Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.

Zaburi 19:10

Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.

Zaburi 19:11

Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.

Zaburi 19:12

Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri.

Zaburi 19:13

Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.

Zaburi 19:14

Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.