Zaburi Mlango 99 Psalms

Zaburi 99:1

Bwana ametamalaki, mataifa wanatetemeka; Ameketi juu ya makerubi, nchi inatikisika.

Zaburi 99:2

Bwana katika Sayuni ni mkuu, Naye ametukuka juu ya mataifa yote.

Zaburi 99:3

Na walishukuru jina lake kuu la kuhofiwa; Ndiye mtakatifu.

Zaburi 99:4

Nguvu za mfalme nazo zapenda hukumu; Wewe ndiwe uliyeithibitisha adili; Ulifanya hukumu na haki katika Yakobo.

Zaburi 99:5

Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni penye kiti cha miguu yake; Ndiye mtakatifu.

Zaburi 99:6

Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia;

Zaburi 99:7

Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao. Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa.

Zaburi 99:8

Ee Bwana, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu; Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe Ingawa uliwapatiliza matendo yao.

Zaburi 99:9

Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.