Zaburi Mlango 104 Psalms

Zaburi 104:1

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama.

Zaburi 104:2

Umejivika nuru kama vazi; Umezitandika mbingu kama pazia;

Zaburi 104:3

Na kuziweka nguzo za orofa zake majini. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, Na kwenda juu ya mabawa ya upepo,

Zaburi 104:4

Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.

Zaburi 104:5

Uliiweka nchi juu ya misingi yake, Isitikisike milele.

Zaburi 104:6

Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi, Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima.

Zaburi 104:7

Kwa kukemea kwako yakakimbia, Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi,

Zaburi 104:8

Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, Mpaka mahali ulipoyatengenezea.

Zaburi 104:9

Umeweka mpaka yasiupite, Wala yasirudi kuifunikiza nchi.

Zaburi 104:10

Hupeleka chemchemi katika mabonde; Zapita kati ya milima;

Zaburi 104:11

Zamnywesha kila mnyama wa kondeni; Punda mwitu huzima kiu yao.

Zaburi 104:12

Kandokando hukaa ndege wa angani; Kati ya matawi hutoa sauti zao.

Zaburi 104:13

Huinywesha milima toka orofa zake; Nchi imeshiba mazao ya kazi zako.

Zaburi 104:14

Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi,

Zaburi 104:15

Na divai imfurahishe mtu moyo wake. Aung'aze uso wake kwa mafuta, Na mkate umburudishe mtu moyo wake.

Zaburi 104:16

Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.

Zaburi 104:17

Ndimo ndege wafanyamo vitundu vyao, Na korongo, misunobari ni nyumba yake.

Zaburi 104:18

Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu, Na magenge ni kimbilio la wibari.

Zaburi 104:19

Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati, Jua latambua kuchwa kwake.

Zaburi 104:20

Wewe hufanya giza, kukawa usiku, Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu.

Zaburi 104:21

Wana-simba hunguruma wakitaka mawindo, Ili kutafuta chakula chao kwa Mungu.

Zaburi 104:22

Jua lachomoza, wanakwenda zao, Na kujilaza mapangoni mwao.

Zaburi 104:23

Mwanadamu atoka kwenda zake kazini, Na kwenye utumishi wake mpaka jioni.

Zaburi 104:24

Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.

Zaburi 104:25

Bahari iko kule, kubwa na upana, Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika, Viumbe hai vidogo kwa vikubwa.

Zaburi 104:26

Ndimo zipitamo merikebu, Ndimo alimo lewiathani uliyemwumba acheze humo.

Zaburi 104:27

Hao wote wanakungoja Wewe, Uwape chakula chao kwa wakati wake.

Zaburi 104:28

Wewe huwapa, Wao wanakiokota; Wewe waukunjua mkono wako, Wao wanashiba mema;

Zaburi 104:29

Wewe wauficha uso wako, Wao wanafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao,

Zaburi 104:30

Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi.

Zaburi 104:31

Utukufu wa Bwana na udumu milele; Bwana na ayafurahie matendo yake.

Zaburi 104:32

Aitazama nchi, inatetemeka; Aigusa milima, inatoka moshi.

Zaburi 104:33

Nitamwimbia Bwana maadamu ninaishi; Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai;

Zaburi 104:34

Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia Bwana.

Zaburi 104:35

Wenye dhambi waangamizwe katika nchi, Watendao ubaya wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.