Zaburi Mlango 107 Psalms

Zaburi 107:1

Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Zaburi 107:2

Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.

Zaburi 107:3

Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

Zaburi 107:4

Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa.

Zaburi 107:5

Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.

Zaburi 107:6

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

Zaburi 107:7

Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.

Zaburi 107:8

Na wamshukuru Bwana, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

Zaburi 107:9

Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema.

Zaburi 107:10

Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,

Zaburi 107:11

Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu.

Zaburi 107:12

Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.

Zaburi 107:13

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

Zaburi 107:14

Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao.

Zaburi 107:15

Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

Zaburi 107:16

Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.

Zaburi 107:17

Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.

Zaburi 107:18

Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti.

Zaburi 107:19

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

Zaburi 107:20

Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.

Zaburi 107:21

Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

Zaburi 107:22

Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.

Zaburi 107:23

Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi,

Zaburi 107:24

Hao huziona kazi za Bwana, Na maajabu yake vilindini.

Zaburi 107:25

Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake.

Zaburi 107:26

Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya.

Zaburi 107:27

Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea.

Zaburi 107:28

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

Zaburi 107:29

Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza.

Zaburi 107:30

Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani.

Zaburi 107:31

Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

Zaburi 107:32

Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee.

Zaburi 107:33

Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu.

Zaburi 107:34

Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa.

Zaburi 107:35

Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.

Zaburi 107:36

Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa.

Zaburi 107:37

Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.

Zaburi 107:38

Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao.

Zaburi 107:39

Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni.

Zaburi 107:40

Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.

Zaburi 107:41

Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo.

Zaburi 107:42

Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.

Zaburi 107:43

Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana.