Zaburi Mlango 76 Psalms

Zaburi 76:1

Katika Yuda Mungu amejulikana, Katika Israeli jina lake ni kuu.

Zaburi 76:2

Kibanda chake pia kiko Salemu, Na maskani yake iko Sayuni.

Zaburi 76:3

Huko ndiko alikoivunja mishale ya uta, Ngao, na upanga, na zana za vita.

Zaburi 76:4

Wewe U mwenye fahari na adhama, Toka milima ya mateka.

Zaburi 76:5

Wametekwa wenye moyo thabiti; Wamelala usingizi; Wala hawakuiona mikono yao Watu wote walio hodari.

Zaburi 76:6

Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, Gari na farasi wameshikwa na usingizi mzito.

Zaburi 76:7

Wewe ndiwe utishaye, naam, Wewe; Naye ni nani awezaye kusimama ufanyapo hasira?

Zaburi 76:8

Toka mbinguni ulitangaza hukumu; Nchi iliogopa, ikakaa kimya.

Zaburi 76:9

Mungu aliposimama ili kuhukumu Na kuwaokoa wapole wa dunia wote pia.

Zaburi 76:10

Maana hasira ya binadamu itakusifu, Masalio ya hasira utajifunga kama mshipi.

Zaburi 76:11

Wekeni nadhiri, mkaziondoe Kwa Bwana, Mungu wenu. Wote wanaomzunguka wamletee hedaya, Yeye astahiliye kuogopwa.

Zaburi 76:12

Yeye huzikata roho za wakuu; Na kuwatisha wafalme wa dunia.