Zaburi Mlango 25 Psalms

Zaburi 25:1

Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu,

Zaburi 25:2

Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.

Zaburi 25:3

Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu.

Zaburi 25:4

Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako,

Zaburi 25:5

Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa.

Zaburi 25:6

Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani.

Zaburi 25:7

Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana kwa ajili ya wema wako.

Zaburi 25:8

Bwana yu mwema, mwenye adili, Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.

Zaburi 25:9

Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake.

Zaburi 25:10

Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.

Zaburi 25:11

Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi.

Zaburi 25:12

Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua.

Zaburi 25:13

Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa; Wazao wake watairithi nchi.

Zaburi 25:14

Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.

Zaburi 25:15

Macho yangu humwelekea Bwana daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.

Zaburi 25:16

Uniangalie na kunifadhili, Maana mimi ni mkiwa na mteswa.

Zaburi 25:17

Katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, Na kunitoa katika dhiki zangu.

Zaburi 25:18

Utazame teso langu na taabu yangu; Unisamehe dhambi zangu zote.

Zaburi 25:19

Uwatazame adui zangu, maana ni wengi, Wananichukia kwa machukio ya ukali.

Zaburi 25:20

Unilinde nafsi yangu na kuniponya, Nisiaibike, maana nakukimbilia Wewe.

Zaburi 25:21

Ukamilifu na unyofu zinihifadhi, Maana nakungoja Wewe.

Zaburi 25:22

Ee Mungu, umkomboe Israeli, Katika taabu zake zote.