Zaburi Mlango 147 Psalms

Zaburi 147:1

Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.

Zaburi 147:2

Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.

Zaburi 147:3

Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao.

Zaburi 147:4

Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina.

Zaburi 147:5

Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka.

Zaburi 147:6

Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri.

Zaburi 147:7

Mwimbieni Bwana kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi.

Zaburi 147:8

Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuyameesha majani milimani.

Zaburi 147:9

Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.

Zaburi 147:10

Hapendezwi na nguvu za farasi, Wala hairidhii miguu ya mtu.

Zaburi 147:11

Bwana huwaridhia wao wamchao, Na kuzitarajia fadhili zake.

Zaburi 147:12

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.

Zaburi 147:13

Maana ameyakaza mapingo ya malango yako, Amewabariki wanao ndani yako.

Zaburi 147:14

Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, Akushibishaye kwa unono wa ngano.

Zaburi 147:15

Huipeleka amri yake juu ya nchi, Neno lake lapiga mbio sana.

Zaburi 147:16

Ndiye atoaye theluji kama sufu, Huimwaga barafu yake kama majivu,

Zaburi 147:17

Hutupa mvua ya mawe kama makombo, Mbele ya baridi yake ni nani awezaye kusimama?

Zaburi 147:18

Hulituma neno lake na kuviyeyusha, Huuvumisha upepo wake, maji yakatiririka.

Zaburi 147:19

Humhubiri Yakobo neno lake, Na Israeli amri zake na hukumu zake.

Zaburi 147:20

Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, Wala hukumu zake hawakuzijua. Haleluya.