Zaburi Mlango 51 Psalms

Zaburi 51:1

Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu.

Zaburi 51:2

Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.

Zaburi 51:3

Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.

Zaburi 51:4

Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.

Zaburi 51:5

Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.

Zaburi 51:6

Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,

Zaburi 51:7

Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji

Zaburi 51:8

Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi.

Zaburi 51:9

Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.

Zaburi 51:10

Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu

Zaburi 51:11

Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

Zaburi 51:12

Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.

Zaburi 51:13

Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako.

Zaburi 51:14

Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako.

Zaburi 51:15

Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako.

Zaburi 51:16

Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.

Zaburi 51:17

Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

Zaburi 51:18

Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu.

Zaburi 51:19

Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako.