Zaburi Mlango 106 Psalms

Zaburi 106:1

Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Zaburi 106:2

Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana, Kuzihubiri sifa zake zote?

Zaburi 106:3

Heri washikao hukumu, Na kutenda haki sikuzote.

Zaburi 106:4

Ee Bwana, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. Unijilie kwa wokovu wako,

Zaburi 106:5

Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako.

Zaburi 106:6

Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu, Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.

Zaburi 106:7

Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu.

Zaburi 106:8

Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu.

Zaburi 106:9

Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda.

Zaburi 106:10

Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao.

Zaburi 106:11

Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao.

Zaburi 106:12

Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake.

Zaburi 106:13

Wakayasahau matendo yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake.

Zaburi 106:14

Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani.

Zaburi 106:15

Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao.

Zaburi 106:16

Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa Bwana.

Zaburi 106:17

Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu.

Zaburi 106:18

Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya.

Zaburi 106:19

Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.

Zaburi 106:20

Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani.

Zaburi 106:21

Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri.

Zaburi 106:22

Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.

Zaburi 106:23

Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.

Zaburi 106:24

Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake.

Zaburi 106:25

Bali wakanung'unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya Bwana.

Zaburi 106:26

Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani,

Zaburi 106:27

Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali.

Zaburi 106:28

Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu.

Zaburi 106:29

Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia.

Zaburi 106:30

Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa.

Zaburi 106:31

Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele.

Zaburi 106:32

Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao,

Zaburi 106:33

Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.

Zaburi 106:34

Hawakuwaharibu watu wa nchi Kama Bwana alivyowaambia;

Zaburi 106:35

Bali walijichanganya na mataifa, Wakajifunza matendo yao.

Zaburi 106:36

Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao.

Zaburi 106:37

Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.

Zaburi 106:38

Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu.

Zaburi 106:39

Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao.

Zaburi 106:40

Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake.

Zaburi 106:41

Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala.

Zaburi 106:42

Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao.

Zaburi 106:43

Mara nyingi aliwaponya, Bali walikuwa wakimwasi kwa mashauri yao, Wakadhilika katika uovu wao.

Zaburi 106:44

Lakini aliyaangalia mateso yao, Aliposikia kilio chao.

Zaburi 106:45

Akawakumbukia agano lake; Akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake;

Zaburi 106:46

Akawajalia kuhurumiwa Na watu wote waliowateka.

Zaburi 106:47

Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako.

Zaburi 106:48

Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Watu wote na waseme, Amina. Haleluya.