Zaburi Mlango 29 Psalms

Zaburi 29:1

Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu;

Zaburi 29:2

Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.

Zaburi 29:3

Sauti ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji mengi.

Zaburi 29:4

Sauti ya Bwana ina nguvu; Sauti ya Bwana ina adhama;

Zaburi 29:5

Sauti ya Bwana yaivunja mierezi; Naam, Bwana aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni;

Zaburi 29:6

Airusha-rusha kama ndama wa ng'ombe; Lebanoni na Sirioni kama mwana-nyati.

Zaburi 29:7

Sauti ya Bwana yaipasua miali ya moto;

Zaburi 29:8

Sauti ya Bwana yalitetemesha jangwa; Bwana alitetemesha jangwa la Kadeshi.

Zaburi 29:9

Sauti ya Bwana yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu.

Zaburi 29:10

Bwana aliketi juu ya Gharika; Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele.

Zaburi 29:11

Bwana atawapa watu wake nguvu; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.