Zaburi Mlango 50 Psalms

Zaburi 50:1

Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake.

Zaburi 50:2

Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika.

Zaburi 50:3

Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote.

Zaburi 50:4

Ataziita mbingu zilizo juu, Na nchi pia awahukumu watu wake.

Zaburi 50:5

Nikusanyieni wacha Mungu wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.

Zaburi 50:6

Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.

Zaburi 50:7

Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena, Mimi nitakushuhudia, Israeli; Mimi ndimi niliye MUNGU, Mungu wako.

Zaburi 50:8

Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako, Na kafara zako ziko mbele zangu daima.

Zaburi 50:9

Sitatwaa ng'ombe katika nyumba yako, Wala beberu katika mazizi yako.

Zaburi 50:10

Maana kila hayawani ni wangu, Na makundi juu ya milima elfu.

Zaburi 50:11

Nawajua ndege wote wa milima, Na wanyama wote wa mashamba ni wangu

Zaburi 50:12

Kama ningekuwa na njaa singekuambia, Maana ulimwengu ni wangu, navyo viujazavyo.

Zaburi 50:13

Je! Nile nyama ya mafahali! Au ninywe damu ya mbuzi!

Zaburi 50:14

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.

Zaburi 50:15

Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.

Zaburi 50:16

Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?

Zaburi 50:17

Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

Zaburi 50:18

Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.

Zaburi 50:19

Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.

Zaburi 50:20

Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.

Zaburi 50:21

Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.

Zaburi 50:22

Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.

Zaburi 50:23

Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.