Zaburi Mlango 92 Psalms

Zaburi 92:1

Ni neno jema kumshukuru Bwana, Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.

Zaburi 92:2

Kuzitangaza rehema zako asubuhi, Na uaminifu wako wakati wa usiku.

Zaburi 92:3

Kwa chombo chenye nyuzi kumi, Na kwa kinanda, Na kwa mlio wa kinubi.

Zaburi 92:4

Kwa kuwa umenifurahisha, Bwana, Kwa kazi yako; nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.

Zaburi 92:5

Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.

Zaburi 92:6

Mtu mjinga hayatambui hayo, Wala mpumbavu hayafahamu.

Zaburi 92:7

Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;

Zaburi 92:8

Bali Wewe, Bwana, U Mtukufu hata milele.

Zaburi 92:9

Maana hao adui zako, Ee Bwana, Hao adui zako watapotea, Na watendao maovu watatawanyika wote pia.

Zaburi 92:10

Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati, Nimepakwa mafuta mabichi.

Zaburi 92:11

Na jicho langu limewatazama walioniotea, Sikio langu limesikia habari za waovu walionishambulia.

Zaburi 92:12

Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.

Zaburi 92:13

Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.

Zaburi 92:14

Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.

Zaburi 92:15

Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.