Zaburi Mlango 69 Psalms

Zaburi 69:1

Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu.

Zaburi 69:2

Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha.

Zaburi 69:3

Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu wangu.

Zaburi 69:4

Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.

Zaburi 69:5

Ee Mungu, unajua upumbavu wangu, Wala hukufichwa dhambi yangu.

Zaburi 69:6

Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe, Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi. Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe, Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.

Zaburi 69:7

Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.

Zaburi 69:8

Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.

Zaburi 69:9

Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.

Zaburi 69:10

Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.

Zaburi 69:11

Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.

Zaburi 69:12

Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.

Zaburi 69:13

Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.

Zaburi 69:14

Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.

Zaburi 69:15

Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze, Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.

Zaburi 69:16

Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.

Zaburi 69:17

Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi.

Zaburi 69:18

Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie.

Zaburi 69:19

Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote.

Zaburi 69:20

Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.

Zaburi 69:21

Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.

Zaburi 69:22

Meza yao mbele yao na iwe mtego; Naam, wakiwa salama na iwe tanzi.

Zaburi 69:23

Macho yao yatiwe giza wasione, Na viuno vyao uvitetemeshe daima.

Zaburi 69:24

Uimwage ghadhabu yako juu yao, Na ukali wa hasira yako uwapate.

Zaburi 69:25

Matuo yao na yawe ukiwa, Pasiwe na mtu wa kukaa hemani mwao.

Zaburi 69:26

Maana wanamwudhi mtu uliyempiga Wewe, Wanasimulia maumivu ya hao uliowatia jeraha.

Zaburi 69:27

Uwaongezee uovu juu ya uovu, Wala wasiingie katika haki yako.

Zaburi 69:28

Na wafutwe katika chuo cha uhai, Wala pamoja na wenye haki wasiandikwe.

Zaburi 69:29

Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Mungu, wokovu wako utaniinua.

Zaburi 69:30

Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani.

Zaburi 69:31

Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng'ombe, Au ndama mwenye pembe na kwato.

Zaburi 69:32

Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.

Zaburi 69:33

Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake.

Zaburi 69:34

Mbingu na nchi zimsifu, Bahari na vyote viendavyo ndani yake.

Zaburi 69:35

Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda, Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.

Zaburi 69:36

Wazao wa watumishi wake watairithi, Nao walipendao jina lake watakaa humo.