Zaburi Mlango 137 Psalms

Zaburi 137:1

Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.

Zaburi 137:2

Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu.

Zaburi 137:3

Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.

Zaburi 137:4

Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

Zaburi 137:5

Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau.

Zaburi 137:6

Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka. Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu.

Zaburi 137:7

Ee Bwana, uwakumbuke wana wa Edomu, Siku ya Yerusalemu. Waliosema, Bomoeni! Bomoeni hata misingini!

Zaburi 137:8

Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia, Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi.

Zaburi 137:9

Heri yeye atakayewakamata wadogo wako, Na kuwaseta wao juu ya mwamba.