Zaburi Mlango 17 Psalms

Zaburi 17:1

Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.

Zaburi 17:2

Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.

Zaburi 17:3

Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,

Zaburi 17:4

Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.

Zaburi 17:5

Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.

Zaburi 17:6

Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.

Zaburi 17:7

Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.

Zaburi 17:8

Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;

Zaburi 17:9

Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.

Zaburi 17:10

Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno.

Zaburi 17:11

Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.

Zaburi 17:12

Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake.

Zaburi 17:13

Ee Bwana, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya.

Zaburi 17:14

Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,

Zaburi 17:15

Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.