Zaburi Mlango 88 Psalms

Zaburi 88:1

Ee Bwana, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako.

Zaburi 88:2

Maombi yangu yafike mbele zako, Uutegee ukelele wangu sikio lako.

Zaburi 88:3

Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu.

Zaburi 88:4

Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada.

Zaburi 88:5

Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.

Zaburi 88:6

Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini.

Zaburi 88:7

Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote.

Zaburi 88:8

Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka.

Zaburi 88:9

Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso Bwana, nimekuita kila siku; Nimekunyoshea Wewe mikono yangu.

Zaburi 88:10

Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi?

Zaburi 88:11

Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu?

Zaburi 88:12

Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?

Zaburi 88:13

Lakini mimi nimekulilia Wewe, Bwana, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia.

Zaburi 88:14

Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako?

Zaburi 88:15

Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika.

Zaburi 88:16

Hasira zako kali zimepita juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza.

Zaburi 88:17

Yamenizunguka kama maji mchana kutwa, Yamenisonga yote pamoja.

Zaburi 88:18

Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo gizani.