Zaburi Mlango 57 Psalms

Zaburi 57:1

Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.

Zaburi 57:2

Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.

Zaburi 57:3

Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake

Zaburi 57:4

Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.

Zaburi 57:5

Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.

Zaburi 57:6

Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake!

Zaburi 57:7

Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi,

Zaburi 57:8

Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.

Zaburi 57:9

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.

Zaburi 57:10

Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni.

Zaburi 57:11

Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.