Zaburi Mlango 1 Psalms

Zaburi 1:1

Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

Zaburi 1:2

Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

Zaburi 1:3

Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.

Zaburi 1:4

Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

Zaburi 1:5

Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki.

Zaburi 1:6

Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.