Zaburi Mlango 144 Psalms

Zaburi 144:1

Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana.

Zaburi 144:2

Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu.

Zaburi 144:3

Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie?

Zaburi 144:4

Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho.

Zaburi 144:5

Bwana, uziinamishe mbingu zako, ushuke, Uiguse milima nayo itatoka moshi.

Zaburi 144:6

Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe.

Zaburi 144:7

Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, katika mkono wa wageni.

Zaburi 144:8

Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.

Zaburi 144:9

Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.

Zaburi 144:10

Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu.

Zaburi 144:11

Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.

Zaburi 144:12

Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu.

Zaburi 144:13

Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu.

Zaburi 144:14

Ng'ombe zetu na wachukue mizigo, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu.

Zaburi 144:15

Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye Bwana kuwa Mungu wao.