Zaburi Mlango 94 Psalms

Zaburi 94:1

Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze,

Zaburi 94:2

Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao.

Zaburi 94:3

Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?

Zaburi 94:4

Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi?

Zaburi 94:5

Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako;

Zaburi 94:6

Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima.

Zaburi 94:7

Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.

Zaburi 94:8

Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?

Zaburi 94:9

Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?

Zaburi 94:10

Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue?

Zaburi 94:11

Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.

Zaburi 94:12

Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako;

Zaburi 94:13

Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.

Zaburi 94:14

Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake,

Zaburi 94:15

Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.

Zaburi 94:16

Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu?

Zaburi 94:17

Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya.

Zaburi 94:18

Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.

Zaburi 94:19

Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu.

Zaburi 94:20

Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria?

Zaburi 94:21

Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia.

Zaburi 94:22

Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia.

Zaburi 94:23

Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza.