Zaburi Mlango 36 Psalms

Zaburi 36:1

Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.

Zaburi 36:2

Kwa maana hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa.

Zaburi 36:3

Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema.

Zaburi 36:4

Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii.

Zaburi 36:5

Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni, Uaminifu wako hata mawinguni.

Zaburi 36:6

Haki yako ni kama milima ya Mungu, Hukumu zako ni vilindi vikuu, Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.

Zaburi 36:7

Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhili zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.

Zaburi 36:8

Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako, Nawe utawanywesha mto wa furaha zako.

Zaburi 36:9

Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru.

Zaburi 36:10

Uwadumishie wakujuao fadhili zako, Na wanyofu wa moyo uaminifu wako.

Zaburi 36:11

Mguu wa kiburi usinikaribie, Wala mkono wa wasio haki usinifukuze.

Zaburi 36:12

Huko ndiko walikoanguka wafanyao maovu; Wameangushwa chini wasiweze kusimama.