Zaburi Mlango 66 Psalms

Zaburi 66:1

Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,

Zaburi 66:2

Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake.

Zaburi 66:3

Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, Adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako.

Zaburi 66:4

Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, Naam, italiimbia jina lako.

Zaburi 66:5

Njoni yatazameni matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu;

Zaburi 66:6

Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; Katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko mlikomfurahia.

Zaburi 66:7

Atawala kwa uweza wake milele; Macho yake yanaangalia mataifa; Waasio wasijitukuze nafsi zao.

Zaburi 66:8

Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu, Itangazeni sauti ya sifa zake;

Zaburi 66:9

Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai, Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.

Zaburi 66:10

Kwa maana umetupima, Ee Mungu, Umetujaribu inavyojaribiwa fedha.

Zaburi 66:11

Ulituingiza ndani ya wavu, Na kuweka viunoni mwetu mzigo uliotulemea.

Zaburi 66:12

Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipita motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kunako wingi.

Zaburi 66:13

Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu;

Zaburi 66:14

Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni.

Zaburi 66:15

Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi.

Zaburi 66:16

Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.

Zaburi 66:17

Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu.

Zaburi 66:18

Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia.

Zaburi 66:19

Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu.

Zaburi 66:20

Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.