Zaburi Mlango 55 Psalms

Zaburi 55:1

Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.

Zaburi 55:2

Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua.

Zaburi 55:3

Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi.

Zaburi 55:4

Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia.

Zaburi 55:5

Hofu na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza.

Zaburi 55:6

Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe.

Zaburi 55:7

Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani.

Zaburi 55:8

Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.

Zaburi 55:9

Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.

Zaburi 55:10

Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo ndani yake;

Zaburi 55:11

Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.

Zaburi 55:12

Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione.

Zaburi 55:13

Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.

Zaburi 55:14

Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.

Zaburi 55:15

Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.

Zaburi 55:16

Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa;

Zaburi 55:17

Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.

Zaburi 55:18

Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu, Maana walioshindana nami walikuwa wengi.

Zaburi 55:19

Mungu atasikia na kuwajibu; Ndiye Yeye akaaye tangu milele. Mageuzi ya mambo hayawapati hao, Kwa hiyo hawamchi Mungu.

Zaburi 55:20

Amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye, Amelihalifu agano lake.

Zaburi 55:21

Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi.

Zaburi 55:22

Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.

Zaburi 55:23

Nawe, Ee Mungu, utawatelemsha, Walifikilie shimo la uharibifu; Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao, Bali mimi nitakutumaini Wewe.