Zaburi Mlango 9 Psalms

Zaburi 9:1

Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;

Zaburi 9:2

Nitafurahi na kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.

Zaburi 9:3

Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako.

Zaburi 9:4

Kwa maana umenifanyia hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki.

Zaburi 9:5

Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele;

Zaburi 9:6

Adui wamekoma na kuachwa ukiwa milele. Nayo miji yao uliing'oa; Hata kumbukumbu lao limepotea.

Zaburi 9:7

Bali Bwana atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.

Zaburi 9:8

Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili.

Zaburi 9:9

Bwana atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida.

Zaburi 9:10

Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, Bwana hukuwaacha wakutafutao.

Zaburi 9:11

Mwimbieni Bwana akaaye Sayuni, Yatangazeni kati ya watu matendo yake.

Zaburi 9:12

Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge.

Zaburi 9:13

Wewe, Bwana, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti,

Zaburi 9:14

Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako.

Zaburi 9:15

Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.

Zaburi 9:16

Bwana amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake.

Zaburi 9:17

Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

Zaburi 9:18

Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.

Zaburi 9:19

Bwana, usimame, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako.

Zaburi 9:20

Bwana, uwawekee kitisho, Mataifa na wajijue kuwa ni binadamu.