Zaburi Mlango 18 Psalms

Zaburi 18:1

Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;

Zaburi 18:2

Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.

Zaburi 18:3

Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.

Zaburi 18:4

Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.

Zaburi 18:5

Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili.

Zaburi 18:6

Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.

Zaburi 18:7

Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu.

Zaburi 18:8

Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala, Makaa yakawashwa nao.

Zaburi 18:9

Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.

Zaburi 18:10

Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo.

Zaburi 18:11

Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni.

Zaburi 18:12

Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Mvua ya mawe na makaa ya moto.

Zaburi 18:13

Bwana alipiga radi mbinguni, Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto.

Zaburi 18:14

Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya.

Zaburi 18:15

Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee Bwana, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.

Zaburi 18:16

Alipeleka kutoka juu akanishika, Na kunitoa katika maji mengi.

Zaburi 18:17

Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.

Zaburi 18:18

Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini Bwana alikuwa tegemeo langu.

Zaburi 18:19

Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.

Zaburi 18:20

Bwana alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa.

Zaburi 18:21

Maana nimezishika njia za Bwana, Wala sikumwasi Mungu wangu.

Zaburi 18:22

Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikujiepusha nazo.

Zaburi 18:23

Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu.

Zaburi 18:24

Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.

Zaburi 18:25

Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;

Zaburi 18:26

Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi.

Zaburi 18:27

Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili.

Zaburi 18:28

Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; Bwana Mungu wangu aniangazia giza langu.

Zaburi 18:29

Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.

Zaburi 18:30

Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya Bwana imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia.

Zaburi 18:31

Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu?

Zaburi 18:32

Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu.

Zaburi 18:33

Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.

Zaburi 18:34

Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.

Zaburi 18:35

Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kuume umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza.

Zaburi 18:36

Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza.

Zaburi 18:37

Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe.

Zaburi 18:38

Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu.

Zaburi 18:39

Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita, Hunitiishia chini yangu walioniondokea.

Zaburi 18:40

Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali.

Zaburi 18:41

Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita Bwana lakini hakuwajibu,

Zaburi 18:42

Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani.

Zaburi 18:43

Umeniokoa na mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia.

Zaburi 18:44

Kwa kusikia tu habari zangu, Mara wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea.

Zaburi 18:45

Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka.

Zaburi 18:46

Bwana ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu;

Zaburi 18:47

Ndiye Mungu anipatiaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu.

Zaburi 18:48

Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu wa jeuri.

Zaburi 18:49

Basi, Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.

Zaburi 18:50

Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake,Daudi na mzao wake hata milele.