Zaburi Mlango 39 Psalms

Zaburi 39:1

Nalisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu.

Zaburi 39:2

Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi.

Zaburi 39:3

Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nalisema kwa ulimi wangu,

Zaburi 39:4

Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu.

Zaburi 39:5

Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.

Zaburi 39:6

Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.

Zaburi 39:7

Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana? Matumaini yangu ni kwako.

Zaburi 39:8

Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu.

Zaburi 39:9

Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.

Zaburi 39:10

Uniondolee pigo lako; Kwa uadui wa mkono wako nimeangamia.

Zaburi 39:11

Ukimrudi mtu kwa kumkemea kwa uovu wake, Watowesha uzuri wake kama nondo. Kila mwanadamu ni ubatili.

Zaburi 39:12

Ee Bwana, usikie maombi yangu, Utege sikio lako niliapo, Usiyanyamalie machozi yangu. Kwa maana mimi ni mgeni wako, Msafiri kama baba zangu wote.

Zaburi 39:13

Uniachilie nikunjuke uso, Kabla sijaondoka nisiwepo tena.